Wednesday, February 27, 2013

MIKABALA YA FONOLOJIA

DONDOO UTANGUIZI • Maana ya Fonolojia KIINI • Mikabala mbalambali ya kifonolojia HITIMISHO MAREJELEO Kietimolojia, neno Fonolojia limetokana na maneno mawili ya Kigiriki ambayo ni foni au phone na logos. Foni likiwa na maana ya sauti au uneni na logos inamaanisha stadi au taaluma ya lugha mahususi. Taaluma hii inajikita katika kushughulikia hasa sauti zile ambazo hutumika katika kutofautisha maana za maneno katika lugha mahususi. Fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za binadamu.(Maganga, 1980) Fonolojia ni tawi la isimu ambalo hushughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti zinazotumiwa katika mfumo fulani. (TUKI, 1990) Fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha ya binadamu.(Massamba na wenzake, 2004) Fonolojia ni utanzu wa isimu unaochunguza jinsi sauti za lugha zinavyofanya kazi katika lugha mbalimbali. Fonolojia hushughulikia jinsi sauti hizi zinavyotumika, zinavyounganishwa na kupangwa katika lugha yoyote mahsusi ili kuunda tungo zenye maana. (Habwe na Kalanje, 2004) Kwa ujumla Fonolojia ni taaluma ya isimu ya lugha inayoshughulikia sauti za lugha husika kwa kuchunguza mahusiano na maathiriano ya sauti hizo. Katika Fonolojia kuna mikabala mbalimbali ambayo hujishughulisha na uchanganuzi wa sauti za lugha mahususi, mikabala hiyo ni kama vile Fonolojia arudhi(vipande sauti), Fonolojia asilia zalishi, Fonolojia zalishi, Fonolojia mizani, Fonolojia vipande sauti, Fonolojia vipande sauti huru, Fonolojia leksika na Fonolojia asilia. Fonolojia arudhi ni mkabala wa Fonolojia ambao hushughulikia sauti za binadamu ambazo hubainishwa kwa vipashio au vipengele kama vile toni, kidatu, kiimbo, shada, mkazo, lafudhi na nyingine. Mkazo ni utamkaji wa nguvu zaidi katika sehemu ya neno au fungu la maneno. Utamkaji huu wa nguvu hufanywa katika silabi, hivyo silabi inayotamkwa kwa mkazo ina msikiko mkubwa zaidi kuliko silabi nyingine za neno hilo hilo. Mkazo pia huweza kutumika kubainisha maana tofauti za maneno hasa yale maneno yanayofanana kimaumbo mfano neno ‘barabara’ Baraba′ra (njia kuu) bara′bara (sawa sawa au sawa kabisa) Pia zipo lugha nyingine duniani ambazo zina jozi za maneno zinazotofautishwa kwa mkazo tu. Mfano, katika lugha ya Kirusi neno ‘zamok’ laweza kuwa na maana mbili. Zamok (hekalu) Za’mok (kufuli) Kiimbo ni utaratibu maalumu wa upandaji na ushukaji mawimbi ya sauti katika usemaji wa lugha. (Massamba na wenzake, 2004). Kiimbo pia ni sifa inayobainika katika sentensi nzima na wala si katika neno kama ilivyo katika toni. Kiimbo kinatusaidia kubaini lengo la msemaji kama anatoa maelezo, anauliza swali, anatoa amri au mshangao. Mfano, Baba atafika leo. (maelezo) Baba atafika leo? (swali) Baba atafika leo! (mshangao) Ondokeni hapa. (amri) Pia katika Fonolojia arudhi kuna silabi ambazo ni kipashio cha kifonolojia kinachohusu matamshi ambacho sauti za lugha hutamkwa mara moja kwa pamoja kama fungu moja linalojitegemea kimatamshi. Muundo wa silabi hubainishwa katika lugha mbalimbali. Mfano, Kiswahili neno (analima)- $a$$na$$li$$ma$ Kinyiha (akulya)- $a$$ku$$lya$ Kingoni (iheka)- $i$$he$$ka$ Lafudhi ni sifa ya kimasikizi ya matamshi ya mtu binafsi ambayo humpa msemaji utambulisho fulani ama wa jamii au kieneo. Lafudhi hujitokeza katika lugha mbalimbali. Mfano, Hero rafiki (msemaji atakuwa Mmasai) Usirete matata mura (msemaji atuwa kutoka Mara) Ninunuliepo ndisi (Mnyakyusa) Mtakuja muje (msemaji atakuwa Mnyiha) Fonolojia asilia zalishi ni mkabala mwingine wa Fonolojia ambao husisitiza zaidi mfumo wa sauti za lugha asilia. Katika kuchunguza mfumo wa sauti asilia husisitiza zaidi muundo wa ndani na muundo wa nje wa lugha asilia. Mfano wa sauti za lugha za asilia ni ule ambao haujafanyiwa uyeyushaji,udondoshaji na zingine. (Massamba, 1996:160) Mfano, umbo la ndani umbo la nje Mu+alimu Mwalimu Mu+ezi Mwezi Mu+aka Mwaka Fonolojia leksika ni mkabala wa kifonolojia ambao hujikita katika kushughulikia neno zima katika uchanganuzi wake. Mkabala huu hauangalii silabi moja au mofimu zinazounda neno hilo bali huangalia neno kwa ujumla wake. Mfano, njoo, ndizi, njia, ndama Maneno haya ukivunjavunja katika vipande sauti hayawezi kuleta maana. (Massamba, 1996:165) Fonolojia mizani ni mkabala wa kifonolojia ambao hujikita katika kushughulikia urefu baina ya silabi moja na nyingine katika utoaji wa sauti. Silabi moja yaweza kutamkwa kwa urefu tofauti mfano neno ‘Haleluya’, ‘Shikamoo’ Miongoni mwa wanaisimu walisawiri katika mkabala ni Levelt (1989), Liberman (1975) na Prince (1977). Pia katika makalaya “Ulemavu wa Usemi na Lugha” Chuo Kikuu Kenyatta, tarehe 24/7/2012.walibaini kuwa kigugumizi kinaweza kuongeza urefu wa silabi katika neno. Opentomatic.com/Sw/Fb/html 27/11/2012 13:05 Mfano neno ‘haleluya’ likitamkwa kwa kigugumizi huweza kusababisha urefu baina ya silabi. Fonolojia vipande sauti ni mkabala ambao hushughulikia uchanganuzi wa sauti za lugha asilia. Mfano, Kiswahili na siyo lugha zilizofanyiwa uundilizi kama vile lugha ya ‘Kiesperanto’. Pia katika mkabala huu huangalia vipashio vya Fonolojia, fonimu na alofoni. Vipande na vipamba sauti huwakilishwa katika mstari mmoja. Mfano, neno ‘amekuja’ linaweza kuwakilishwa kwa namna tofauti tofauti kwa kutumia alama za uandishi kama kiulizo, mshangao,nukta, kama inavyoonesha hapa chini. Amekuja? Amekuja! Amekuja. Fonolojia vipande sauti huru, hushughulikia vipande sauti na vipamba sauti ambavyo hujitegemea katika uwakilishi wake na siyo katika mstari mmoja kama ilivyo katika mkabala wa vipamba sauti. Mfano, Amefau′lu Wu′se Wuse′ Fonolojia zalishi ni mkabala ambao hushughulikia kanuni mbalmbali za kifonolojia na sheria za lugha za kimajumui, kila lugha ina muundo wa sauti za maneno na sentensi zake. Waasisi wa mkabala huu ni Vonnemann(1971-1974), Hooper(1975-1979) na Hudson (1975). Mfano katika lugha ya Kiswahili neno ‘lima’ linaweza kunyumbulishwa kama vile limisha, limiana, limia, limiwa, limwa. Pia katika lugha ya Kiingereza neno ‘produce’ laweza kunyumbulishwa kama vile produced, producer, production. Fonolojia asilia ni mkabala unaohusika zaidi katika lugha ya binadamu inayotumiwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo mawasiliano kwa njia ya sauti zinazounda maneno. Waasisi wa mkabala huu ni David Stampe (1969-1973) ambaye ni wa kwanza kuelezea mkabala huu na baadaye alifuatia na mwasisi mwingine ambaye ni Patricia Donegan (1979). Lugha asilia hutofautiana sana na lugha nyingine kama vile lugha ya ishara ingawa nayo hutumiwa katika mawasiliano ya binadamu lakini haitumii sauti. Mfano, rota (kuota ndoto), kota (kuota moto). Mikabala ya kifonolojia katika lugha mbalimbali utusaidia katika matumizi ya lugha yoyote ile kwa kutambua msemaji anatoka wapi na ni nani, kujua asili ya maneno yaliyopo katika lugha ya Kiswahili na muundo wa maneno katika lugha. Hivyo hatuna budi kujifunza mikabala ya kifonolojia ambayo itatupa msingi mzuri katika matumizi ya lugha. MAREJELEO Habwe, J. na Karanje, P (2004), Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, Phoenix Publishers Ltd, Nairobi Kipacha, A (2007), Utangulizi wa Lugha na Isimu, Chuo Kikuu cha Tanzania, Dar es Salaam Maganga,C (1980), Kiswahili Vyuoni, Taasisi ya Ukuzaji Mtaala, Dar es Salaam Massamba, D.P.B (1996), Phonological Theory: History and Development, Dar es Salaam University Press, Dar es Salaam Massamba na wenzake (2004), Fonolojia ya Kiswahili Sanifu: Sekondari na Vyuo(FOKISA), Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), Dar es salaam Mgullu, R.S (1999), Mtalaa wa Isimu, Longhorn Publisher(U) Ltd, Kampala Opentomatic.com/Sw/Fb/html 27/11/2012 13:05 T UKI (1990), Kamusi Sanifu ya isimu na Lugha, Dar es Salaam University Press, Dar es Salaam